Pata Habari Motomoto za Nje na Ndani ya Nchi kwa njia ya E-mail, Andika E-mail yako hapo chini.


Home » » BIG MARCH "BARCLAYS PREMIER LEAGUE (EPL)"

BIG MARCH "BARCLAYS PREMIER LEAGUE (EPL)"

ARSENAL NA MANCHESTER CITY NI ANA KWA ANA AU USO KWA USO LEO HII PALE MTAA WA EMIRATES NANI ATAIBUKA MSHINDI?



Ligi kuu ya Uingereza inarejea, baada ya mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa za mashindano rasmi na zile za kirafiki katika mabara takriban yote ya dunia. Jumla ya mechi 10 zinatarajiwa kupigwa weekend hii, mechi nane zikipigwa siku ya Jumamosi, na mechi moja moja siku za jumapili na jumatatu. Hata hivyo, mechi kubwa ya weekend itakuwa ile yenye kuzikutanisha Arsenal na Manchester City, mechi ambayo itapigwa katika dimba la Emirates, yaliko maskani ya Arsenal iliyo chini ya kocha Arsene Wenger.

Hii ni moja ya mechi ambazo zimekuwa zikivuta hisia za mashabiki lukuki katika siku za karibuni, kutokana na upinzani ambao umezidi kuimarika baina ya timu hizi mbili. Tayari, Arsenal walishatangaza ubabe kwa City, katika pambano la ngao ya Hisani kwenye mechi ya uzinduzi wa ,msimu huu wa ligi, lakini pambano hili la ligi yenyewe, halitarajiwi kuwa sawa na mechi ile ya hisani.

Danny Welbeck, anapewa nafasi kubwa sana ya kushuka dimbani dhidi ya Manchester City, kwa mara ya kwanza akiwa katika uzi wa Arsenal, kufuatia uhamisho wake wa siku ya mwisho ya usajili, uliogharimu paundi za Uingereza milioni 16. Mchezaji huyu, amekuwa gumzo kubwa sana hivi sasa, kufuatia uhamisho huo, upande mmoja wa mijadala ukiponda rekodi zake katika ufungaji, huku mwingine ukitetea rekodi hizo kwa kile kinachoelezwa kuwa, hakuwahi kupewa nafasi ya kung’ara akiwa United, kufuatia kuchezeshwa zaidi pembeni na si katikati anakoonekana kuwa bora.

Na hoja za upande wa pili zinaonekana kuwa na mshiko, kufuatia mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, kuchezeshwa katikati, mwanzoni mwa wiki wakati kikosi cha Uingereza, kilipoumana na Switzerland, na akafunga mabao mazuri mawili yaliyoisaidia Uingereza, kuanza kampeni za kushiriki michuano ya EURO 2016, kwa mafanikio.

Hata hivyo, Arsenal, huenda wakamkosa kiungo aliyeko katika kiwango bora kabisa cha maisha yake ya soka, Aaron Ramsey, ambaye alionekana kupata maumivu wakati akiitumikia timu ya taifa ya Wales, wiki hii, ingawa Arsenal, wamesema kuwa majeraha yake si makubwa na anaweza kuwa kikosini.

Kwa upande wa wageni katika pambano hilo, Manchester City, huenda wakamkosa mlinzi wao Pablo Zabaleta, ambaye naye alionekana kupata majeraha wakati akiwa timu ya taifa, kama ilivyo kwa mshambuliaji Stevan Jovetic. Na huu utakuwa mwanzo wa mechi ngumu tatu kwa kikosi cha Manuel Pellegrini, ambaye baada ya mechi ya ugenini dhidi ya Arsenal, ana mechi ya ugenini dhidi ya Bayern Munich katika michuano ya Ligi ya mabingwa na kisha Chelsea katika mechi ya ligi.

Ni mtihani mgumu, lakini ambao wengi wanaamini utatoa uelekeo wa uimara wa kikosi hiki katika msimu huu.

DONDOO MUHIMU ZA PAMBANO HILI::
Kihistoria, Arsenal wameshinda mechi 52 za nyumbani kwao, dhidi ya City, wakipoteza 14 na sare 20, ingawa takwimu za mechi za karibuni zinaonyesha kuwa Arsenal wameshinda mechi moja tu kati ya tano za hivi karibuni, wakitoka sare mechi tatu na kupoteza mechi moja.

Arsenal pia waliwahi kushinda mechi 18 kati ya mechi 22 dhidi ya City hapo awali, lakini ikaambulia kushinda mechi tatu tu katika mechi 12 za hivi karibuni. Lakini jambo jingine lililo zuri kwa Arsenal ni kuwa, hawajapoteza mechi ya nyumbani tangu walipofanya hivyo mara ya mwisho katika siku ya ufunguzi msimu uliopita.

Kwa upande wa City, rekodi zinaonyesha kuwa wamepoteza mechi mbili tu kati ya mechi tisa walizocheza dhidi ya Arsenal hivi karibuni. Aidha, City, ambao walipoteza pambano lao lililopita, hawajawahi poteza mechi mbili mfululizo za ligi tangu walipofanya hivyo mara ya mwisho mwaka 2010, ambapo moja ya mechi mbili mfululizo walizopoteza ilikuwa dhidi ya Arsenal.

Kwa Arsenal, hili ni pambano la kudhihirisha kuwa wako ngangari msimu huu, baada ya usajili wa Alexis Sanches, Calum Chambers na Danny Welbeck. Ni pambano la kuanza kuonyesha kuwa wanaondoa unyonge wao dhidi ya timu za juu ambazo zimekuwa zikiwanyanyasa katika misimu ya karibuni. Lakini Man City nao kwa upande wao, wana mengi ya kuwasukuma kutaka ushindi katika pambano hili, kwahiyo si mechi rahisi hata kidogo.

JE, NI NANJ ATAIBUKA MSHINDI KATIKA PAMBANO HILI?
Unaweza kushiriki kwa kutabiri pambano huu.

Mechi zingine zitakazipigwa weekend hii zitashuhudia Chelsea wakiwakaribisha Swansea, Burnley wakisafiri kwenda kukipiga na Crystal palace huku Southampton wakiwa wenyeji wa Newcastle United. Kwa upande mwingine, Stoke City watakuwa nyumbani wakiwakaribisha Leicester, huku Sunderland nao wakiwa wenyeji wa Tottenham, ilhali West Brom wakishuka kwenye uwanja wao wa nyumbani dhidi ya Everton na Aston Villa wakisafiri kwenda Anfield kuumana na Liverpool.

Siku ya Jumapili, Manchester United watakuwa wakikionyesha kikosi chao ghali sana kwa kukipambanisha na Queens Park Rangers na jumatatu Hull watakuwa wakiwakaribisha WestHam United.

benzema

 

Copyright © 2013. UBUYU KITAANI - Haki zote zimehifadhiwa
Template Modify by Habarizetuleo TEAM
Proudly powered by MAN DUGX